Friday, 30 January 2015

SIMBA WAAMUA KUFANYA MAAMUZI MAGUMU


WAZEE wa Simba wameona isiwe taabu na wameamua kurudi kazini kwa kufanya kikao chao cha dharura na baadhi ya viongozi na jana Alhamisi jioni walituma ujumbe wao kambini kuzungumza na wachezaji kwenye kikao cha faragha kutaka kujua tatizo ni nini mbona timu inayumba?
Lakini si hilo tu, viongozi wa matawi ya Simba Dar es Salaam wameungana na kuuandikia barua uongozi wakishinikiza mambo matatu ambayo ni uamuzi mgumu, ambayo ni kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama kujua tatizo la timu yao, kufumua benchi la ufundi abaki kocha Mserbia, Goran Kopunovic pekee na mwisho Kamati ya Mashindano ipigwe chini.
Wanachama hao chini ya kiongozi wao, Masoud Ustaadh, wanadai kwamba mambo hayo ndiyo tatizo na chanzo cha Simba kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu Bara na kwamba viongozi wa kamati wamekuwa wakiingilia benchi la ufundi.(P.T)
Kwa mujibu wa maelezo yao, wanataka hata Selemani Matola apigwe chini kwa madai kwamba hata Kocha Patrick Phiri alishadokeza awali kuwa Kocha Msaidizi huyo hafai.
Rais wa Simba, Evans Aveva, amekiri kupokea barua hiyo na kusema anaifanyia kazi kwa mujibu wa Katiba ya Simba.
Tafrani hiyo imezuka baada ya timu hiyo kupigwa mabao 2-1 na Mbeya City juzi Jumatano kwenye mechi ya ligi hiyo ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wazee hao waliibukia kambini jana kutaka wachezaji wawaambie ukweli ambapo kikao hicho kilitumia saa kadhaa huku kukiwa na usiri mkubwa.
Mmoja wa wachezaji aliiambia Mwanaspoti baadaye kwamba baadhi yao walitamka kwamba walifungwa kwa makosa ya uwanjani, ingawa wengine walilalamika kuwa morali iko chini kwavile viongozi hawapo karibu nao.
Kocha aliyetimuliwa na Simba, Patrick Phiri kwa upande wake ameweka wazi kwamba timu hiyo ilikosea kuwaacha Amri Kiemba na Haroun Chanongo lakini akatoa angalizo kwamba Mserbia Kopunovic asiguswe, aachwe afanya kazi yake.
Phiri alitimuliwa Simba mwezi uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti jana kutoka Zambia, Phiri alionyesha kusikitishwa na matokeo ya Simba lakini akasema: "Bado uwepo wa Chanongo na Kiemba ndani ya Simba ulikuwa muhimu sana, kila mchezaji ana udhaifu wake kama binadamu, lakini viongozi wanapaswa kukaa na wachezaji kuzungumza nao kujua matatizo yao."
Kiemba alijiunga na Azam kwa mkopo kama Chanongo alivyokwenda Stand United ya Shinyanga.
"Simba haina wachezaji wengi wenye uzoefu, waliopo ni wazuri lakini hakuna umoja wa dhati, bado kuna makundi kwa wachezaji, viongozi waangalie hili kwa kina, ijapokuwa matokeo yanaumiza sana na nimekuwa nikifuatilia Simba kwa karibu," alisema Phiri
"Kwa sasa wasije kufanya kosa la kumfukuza kocha, wakae waangalie wapi kuna tatizo ndani na nje ya timu, bado wana nafasi ya kufanya vizuri bado mechi ni nyingi."
Mzungu amshangaa Chollo
Kopunovic ameshangazwa na tukio la beki mkongwe kuamua kupiga penalti ambayo iliwanyima sare dhidi ya Mbeya City, lakini akatamka kwamba kupoteza mchezo huo ni vizuri kwa sasa kwa sababu itawashtua na kuwarudisha mchezoni kwavile wachezaji walishaanza kujisahau.
"Sawa, sikuwahi kusema nani apige penalti ya kwanza katika mechi zetu, lakini Chollo kupiga penalti lilinishangaza sana kwa kuwa ukiacha mazoezini sikuwahi kumuona akipiga penalti katika mechi lakini sitaki kumlaumu sana," alisema Kopunovic akizungumzia penalti iliyokoswa na Nassor Masoud 'Chollo' na kuipa Mbeya City ushindi wa mabao 2-1.
"Angalia tulivyocheza dakika 30 za mwisho, kwa namna moja nafurahia haya matokeo unajua tangu tuchukue Kombe la Mapinduzi wachezaji wangu walijisahau walikuwa wanajiona wao mastaa wakubwa ni kama wamechukua ubingwa wa ligi, hapa sasa wataamini kuwa safari yao bado ni ndefu."

No comments:

Post a Comment