
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto
(kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo Filikunjombe wakiwa
katika majukumu yao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura (kushoto) akiwa katika majukumu.
KAMATI ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa mapendekezo ya kuinusuru
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kutokana na hali mbaya ya kampuni hiyo
kifedha kwa sasa ambapo inaendeshwa kwa hasara huku ikiwa na madeni
makubwa. PAC imetoa mapendekezo hayo katika taarifa yao kwa bunge ya
mwaka juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mashirika ya umma
iliyotolewa Januari 28 mwaka 2015.
Kwa
mujibu wa taarifa ya PAC hali ya mapato na matumizi ya TTCL kwa mwaka
2012 ilipata hasara ya bilioni 20.883 huku kwa mwaka 2013 ikipata hasara
ya bilioni 16.258. PAC ilisema majumuisho ya hasara ya TTCL kupata
hasara kwa takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na hasara ambayo
kwa mwaka 2013 ilifikia bilioni 334.48, jambo ambalo limeiondolea mvuto
wa kukopeshwa na taasisi za fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.
"...Ukosefu
wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa
TTCL kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi
wa TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Tangu TTCL
ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango
wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na
masharti ya kupata udhamini wa Serikali," ilieleza taarifa hiyo ya PAC.
PAC iliongeza kuwa ukiacha madeni yaliopo pia TTCL inadaiwa na Mamlaka
ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jumla ya bilioni 25 hivyo
kufanya jumla ya deni kufikia bilioni 101.6.
Kamati
hiyo ya bunge imesema kuna umuhimu wa Serikali kufanya maamuzi ya haraka
ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye Sekta ya
Mawasiliano ikizingatiwa kuwa ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa wa
mawasiliano. Katika mapendekezo ya PAC ili kuikwamua TTCL imeishauri
Serikali kununua hisa asilimia 35 zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika
TTCL kwa gharama ndogo kwani Bharti Airtel haikutimiza kikamilifu
masharti ya mkataba wa mauziano ya hisa hizo hapo awali kwani tangu
inunue hisa hizo haijafanya uwekezaji katika Kampuni ya TTCL.
"...TTCL
isamehewe deni la Serikali Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25
bilioni ambayo jumla yake ni Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe
kuongeza mtaji ili Kampuni itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896
bilioni na kuwa na mtaji chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili
basi Kampuni hiyo itaweza kukopesheka. Serikali ikamilishe taratibu
zake za kuimilikisha TTCL Mkongo wa Taifa ili izidi kuuendeleza kwa
ufanisi na kuongeza mapato ya TTCL," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo PAC imeshauri kuwa kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya
muundo wa Kampuni ya TTCL kwani kwa sasa ina idadi kubwa ya wafanyakazi
(1549) isiyoweza kuwalipa.
Aidha,
ilibainisha kuwa kwa sasa zinahitajika bilioni 32 kwa ajili ya
kugharamia urekebishaji wa muundo wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya
utoaji wa huduma mbalimbali. Mashirika mengine yenye hali mbaya kifedha
na uendeshaji ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania, ATCL ambayo kwa
sasa ina madeni makubwa huku ikiwa na ndege moja aina ya Dash 8–Q 300,
Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa Ohio, Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment