Mshtakiwa Tegeta Escrow aachiwa kwa dhamana
![]() |
MSHITAKIWA ESCROW ALIYEACHIWA KWA ZAMANA |
Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabigwa.
Mshtakiwa huyo alitimiza masharti mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi.
Ijumaa iliyopita, Mtabingwa alipandishwa kizimbani na kutakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslim Sh. bilioni moja ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, wadhamini watatu watakaosaini hati ya dhamana ya maandishi ya Sh. milioni 340 kila mmoja, wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi zinazotambulika na kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo na kupelekwa mahabusu hadi jana alipokamilisha hati tano za mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh. bilioni 1.3 na wadhamini watatu, wawili wafanyakazi wa TRA na mmoja mjasiriamali.
Katika kesi ya msingi, Mutabingwa anakabiliwa na mashitaka manne anayodaiwa kutenda Januari 27, 2014 maeneo ya Benki ya Mkombozi iliyopo Manispaa ya Ilala.
Inadaiwa mshtakiwa akiwa katika wadhifa wake wa Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, alipokea rushwa ya Sh. 1, 617,000,000 kupitia akaunti namba 00110202613801 kutoka kwa Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira.
Fedha hizo ni miongoni mwa zilizokuwamo katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Mshtakiwa anadaiwa kupokea tuzo hiyo kwa kuwawakilisha TRA na Mabibo Beer Wines and Spirits inayomilikiwa na Rugemalira.
Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai katika shitaka la pili kuwa, Julai 15, mwaka jana, maeneo ya Benki ya Mkombozi, mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00110202613801, fedha za Escrow kutoka kwa Rugemalira.
Katika shitaka la tatu, inadaiwa kuwa Agosti 26, mwaka jana, maeneo ya Benki ya Mkombozi, mshtakiwa alipokea tena rushwa ya Sh. 161,700,000 kupitia akaunti hiyo hiyo kutoka kwa Rugemalira na fedha hizo zilikuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Swai, alidai katika shitaka la nne kuwa Novemba 14, mwaka jana, kwa kutumia akaunti yake hiyo, alipokea rushwa ya Sh. 161,700,000 kutoka kwa Rugemalira, fedha ambazo zilikuwemo katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Januari 29, mwaka huu
No comments:
Post a Comment