WAZEE wa
Simba wameona isiwe taabu na wameamua kurudi kazini kwa kufanya kikao
chao cha dharura na baadhi ya viongozi na jana Alhamisi jioni walituma
ujumbe wao kambini kuzungumza na wachezaji kwenye kikao cha faragha
kutaka kujua tatizo ni nini mbona timu inayumba?
Lakini si
hilo tu, viongozi wa matawi ya Simba Dar es Salaam wameungana na
kuuandikia barua uongozi wakishinikiza mambo matatu ambayo ni uamuzi
mgumu, ambayo ni kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama kujua tatizo
la timu yao, kufumua benchi la ufundi abaki kocha Mserbia, Goran
Kopunovic pekee na mwisho Kamati ya Mashindano ipigwe chini.
Wanachama
hao chini ya kiongozi wao, Masoud Ustaadh, wanadai kwamba mambo hayo
ndiyo tatizo na chanzo cha Simba kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu Bara na
kwamba viongozi wa kamati wamekuwa wakiingilia benchi la ufundi.(P.T)
Kwa
mujibu wa maelezo yao, wanataka hata Selemani Matola apigwe chini kwa
madai kwamba hata Kocha Patrick Phiri alishadokeza awali kuwa Kocha
Msaidizi huyo hafai.
Rais wa Simba, Evans Aveva, amekiri kupokea barua hiyo na kusema anaifanyia kazi kwa mujibu wa Katiba ya Simba.
Tafrani
hiyo imezuka baada ya timu hiyo kupigwa mabao 2-1 na Mbeya City juzi
Jumatano kwenye mechi ya ligi hiyo ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Wazee hao
waliibukia kambini jana kutaka wachezaji wawaambie ukweli ambapo kikao
hicho kilitumia saa kadhaa huku kukiwa na usiri mkubwa.
Mmoja wa
wachezaji aliiambia Mwanaspoti baadaye kwamba baadhi yao walitamka
kwamba walifungwa kwa makosa ya uwanjani, ingawa wengine walilalamika
kuwa morali iko chini kwavile viongozi hawapo karibu nao.
Kocha
aliyetimuliwa na Simba, Patrick Phiri kwa upande wake ameweka wazi
kwamba timu hiyo ilikosea kuwaacha Amri Kiemba na Haroun Chanongo lakini
akatoa angalizo kwamba Mserbia Kopunovic asiguswe, aachwe afanya kazi
yake.
Phiri alitimuliwa Simba mwezi uliopita na nafasi yake kuchukuliwa na Mserbia huyo.
Akizungumza
na Mwanaspoti jana kutoka Zambia, Phiri alionyesha kusikitishwa na
matokeo ya Simba lakini akasema: "Bado uwepo wa Chanongo na Kiemba ndani
ya Simba ulikuwa muhimu sana, kila mchezaji ana udhaifu wake kama
binadamu, lakini viongozi wanapaswa kukaa na wachezaji kuzungumza nao
kujua matatizo yao."
Kiemba alijiunga na Azam kwa mkopo kama Chanongo alivyokwenda Stand United ya Shinyanga.
"Simba
haina wachezaji wengi wenye uzoefu, waliopo ni wazuri lakini hakuna
umoja wa dhati, bado kuna makundi kwa wachezaji, viongozi waangalie hili
kwa kina, ijapokuwa matokeo yanaumiza sana na nimekuwa nikifuatilia
Simba kwa karibu," alisema Phiri
"Kwa sasa
wasije kufanya kosa la kumfukuza kocha, wakae waangalie wapi kuna
tatizo ndani na nje ya timu, bado wana nafasi ya kufanya vizuri bado
mechi ni nyingi."
Mzungu amshangaa Chollo
Kopunovic
ameshangazwa na tukio la beki mkongwe kuamua kupiga penalti ambayo
iliwanyima sare dhidi ya Mbeya City, lakini akatamka kwamba kupoteza
mchezo huo ni vizuri kwa sasa kwa sababu itawashtua na kuwarudisha
mchezoni kwavile wachezaji walishaanza kujisahau.
"Sawa,
sikuwahi kusema nani apige penalti ya kwanza katika mechi zetu, lakini
Chollo kupiga penalti lilinishangaza sana kwa kuwa ukiacha mazoezini
sikuwahi kumuona akipiga penalti katika mechi lakini sitaki kumlaumu
sana," alisema Kopunovic akizungumzia penalti iliyokoswa na Nassor
Masoud 'Chollo' na kuipa Mbeya City ushindi wa mabao 2-1.
"Angalia
tulivyocheza dakika 30 za mwisho, kwa namna moja nafurahia haya matokeo
unajua tangu tuchukue Kombe la Mapinduzi wachezaji wangu walijisahau
walikuwa wanajiona wao mastaa wakubwa ni kama wamechukua ubingwa wa
ligi, hapa sasa wataamini kuwa safari yao bado ni ndefu."