Sunday, 1 February 2015

Amuua mke kwa kumkata kichwa gesti

1st February 2015
Mkazi wa Tabata Mawenzi, Remi Joseph (36) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kumkata kichwa kwenye nyumba ya wageni ya Friends Corner ya jijini Dar es Salaam.
Aliyeuawa ni Josephena Moshi (35), ambaye alikatwa kichwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani wakiwa kwenye nyumba ya wageni ya Friends Corner.

Akihojiwa kuhusiana na tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa  Kinondoni, Augustine Senga, alikiri kutokea mauaji hayo.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Alhamisi saa 8:00 mchana na kwamba familia hiyo ilikuwa inaishi Tabata Mawenzi.

Senga alisema mwanamke huyo alifariki papo hapo baada ya kushambuliwa na kwamba chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na uchunguzi unaendelea.
Kamanda Senga alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na mtuhumiwa anashikiliwa na polisi.

Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kufanya mauaji hayo, alifanya jaribio la kutaka kujiua lililoshindikana.

Kamanda alipoulizwa kuhusiana na mtuhumiwa huyo kutaka kujiua, alisema kuwa uchunguzi unaendelea.

“Bado ni mapema sana kueleza kila kitu hayo niliyokueleza ni taarifa za awali kwani na huyu mtuhumiwa amekutwa na majeraha shingoni, hivyo masuala ya kazi yake na sababu vinachunguzwa,” alisema Senga.

MKUU WA MKOA AFUNGUA MAFUNZO YA MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII

01_0567b.JPG
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Elimu Zanzibar (ZEDO) Ussi Said Suleiman akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya Social Media huko Chuoni kwao Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar.Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar.
02_ccda3.JPG
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis (alie simama) akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya matumizi ya Mitandao ya kijamii (Social Media), hawapo pichani yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Elimu Zanzibar kwa kushirikiana na Kigamboni Community Centre KCC kutoka Dar es Salam, huko Chuoni kwao Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar.Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar.
03_68a56.JPG
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakimskiliza Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis (hayupo pichani).
04_0d2c4.JPG
Mgeni rasmin Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Khamis (wakatikati) waliokaa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya matumizi ya Mitandao ya kijamii (Social Media).Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar.

SIMBA YAPIGWA FAINI YA MILIONI 3/-

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeipiga klabu ya Simba faini ya sh. milioni tatu kutokana na timu yake kuvaa jezi ambazo hazikuwa na nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom wakati wa mechi yao dhidi ya Kagera Sugar.
Mechi hiyo namba 50 ya Ligi Kuu ya Vodacom ilichezwa Desemba 26 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 13(7) ya Ligi Kuu inayotaka klabu kuheshimu masharti ya udhamini wa Ligi Kuu kwenye mechi zake.
Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni ya 28(4) kwa kusababisha mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati yake na Toto Africans iliyochezwa Januari 14 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuvurugika.
Kutokana na mchezo huo kuvurugika, Toto Africans imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu. Uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia kanuni ya 28(1) inayotawala ligi hiyo